Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Kama tunavyotamani watu watutendee mema, nasi pia tunapaswa kuwatendea mema. Hivyo, iwapo tunataka kuwa waadilifu, tunapaswa kuwatendea watu kama tunavyopenda watutendee.
Riwaya kutoka kwa Imam Hasan al-Mujtaba (a.s):
Ewe mwana wa Adam! Jiepushe na mambo yaliyoharamishwa na Mwenyezi Mungu ili uwe mja wake wa kweli. Ridhika na kile ambacho Mwenyezi Mungu Mtukufu amekugawia ili uwe tajiri (usiye na haja). Fanya wema kwa jirani zako ili uwe Mwislamu wa kweli. Na watendee watu kwa namna ambayo ungependa wakutendee wewe ili uwe mwenye haki.
Mambo manne aliyosisitiza Imam Hasan (a.s):
1. Epuka Maharam (mambo yaliyokatazwa na Mwenyezi Mungu)
Kuabudu kwa maana halisi ni kujiepusha na yale yote ambayo Mwenyezi Mungu ameyaharamisha. Zamani, kupata fursa ya kufanya dhambi haikuwa rahisi kama ilivyo leo. Sasa hivi, vikwazo vya maadili vimepungua na vishawishi vimeongezeka, jambo linalohitaji tahadhari zaidi ili tusipoteze imani yetu. Katika hadithi imeelezwa kwamba, "Kuhifadhi dini katika zama za mwisho ni kama kushikilia moto mkononi."
2. Ridhika na riziki uliyopewa
Ukinyenyekea na kuridhika na sehemu ya riziki aliyokupangia Mwenyezi Mungu, moyo wako utakuwa na utulivu na hautajiona mwenye upungufu. Tatizo la kutoridhika linawafanya watu kukimbilia dunia na kupoteza amani ya ndani. Hali hii imesababisha hata mila nzuri kama kutembeleana (silah rahim) kupungua na mawasiliano ya kijamii kupoteza ukaribu wa zamani.
3. Fanya wema kwa jirani
Mtu anaeheshimu haki za jirani zake ndiye anayehesabika kuwa Mwislamu wa kweli — yaani, yule ambaye Waislamu wenzake wako salama kutokana na ulimi wake na mikono yake. Kwa bahati mbaya, leo hii mara nyingi tunawaona majirani kama watu wa kutushughulikia badala ya sisi kuwashughulikia, na hii hupunguza mshikamano wa kijamii.
4. Watendee watu vile ungependa wakutendee
Hii ndiyo kanuni ya dhahabu ya uadilifu. Ikiwa tungekuwa tunapenda kutendewa kwa heshima, haki na upendo, basi nasi pia tuwape wengine hivyo.
Kauli ya Imam as-Sadiq (a.s) kuhusu Ridhaa:
Ridhaa kwa maamuzi ya Mwenyezi Mungu ni kuridhia yanayopendeza na yasiyopendeza, kwa kuwa ridhaa ni mwanga wa maarifa. Mtu mwenye ridhaa ni yule anayekubali makadirio ya Mwenyezi Mungu bila kuyapinga na ambaye moyo wake unafurahia yale aliyopangiwa na Mola wake.
Vyanzo:
1. Bihar al-Anwar, Juzuu ya 75, uk. 112
2. Man la Yahduruh al-Faqih, Juzuu ya 4, uk. 362
3. Misbah al-Shari‘a, uk. 182.
Your Comment